VODACOM

. MBUNGE wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu (pichani) ataendelea kusota rumande hadi Julai 27, mwaka huu akisubiri uamuzi wa mahakama kuhusu pingamizi la dhamana. Alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana na kusomewa mashitaka ya kutoa lugha ya uchochezi. Mshitakiwa alikana mashitaka hayo na upande wa mashitaka ulidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika. Lissu anayewakilishwa na mawakili 18, alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka ya kutoa lugha ya uchochezi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri. Kurudishwa rumande kwa Lissu kumetokana na upande wa mashitaka kuomba mahakama kupinga dhamana kwa mshitakiwa huku upande wa utetezi ukiiomba mahakama kutoa dhamana. Wakili wa Serikali, Simon Wankyo aliomba mahakama kupinga dhamana ya mshitakiwa kwa kuwa katika mahakama hiyo yapo mashauri manne ambayo ni kesi namba 233/2016, 208/2016, 279/2016 na 123/2017. Wankyo alidai kesi hizo zote zinaashiria mashitaka ya uchochezi na kwamba yamekuwa yakijirudia, ambayo Lissu huyafanya anapoachiwa kwa dhamana mahakamani. Alidai mashitaka hayo yametoka katika uchochezi mpaka kwenye chuki zinazogusa mamlaka mbalimbali za serikali hata usalama wa nchi na sio jambo la kufumbiwa macho. “Haya sio matamshi ya kawaida kwani yatasababisha chuki baina ya Watanzania na mamlaka mbalimbali. Matokeo ya kusababisha chuki sio madogo endapo ataachiwa kwa dhamana kwani yanagusa ukabila, udini na ukanda,” alidai Wankyo. Alisema wanaamini amekuwa akifanya hivyo kwa kuwa yupo nje. Aidha, Wakili wa Serikali, Tumanywa Majigo, alidai mahakama imepewa mamlaka ya kutoa dhamana kwa washitakiwa mbalimbali. Majigo alidai kwa mujibu wa kifungu cha 148 (5) (a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambayo mahakama imepewa mamlaka ya kuzuia dhamana kwa ajili ya ulinzi na usalama wa mshitakiwa na kwamba Lissu akirudi uraiani atadhurika na chuki alizozieneza. Alidai maneno yaliyotolewa yanalenga kubomoa misingi ya umoja na upendo uliojengeka miongoni mwa Watanzania. Hata hivyo, Wakili wa Lissu, Fatma Karume alidai kuwa dhamana ni haki ya mshitakiwa na kwamba upande wa mashitaka wasilazimishe mahakama kumnyima dhamana kwa kuwa hawajakamilisha upelelezi. Karume alidai mahakama itambue kuwa Lissu ni chama cha upinzani na serikali ndio imewakilishwa kuieleza mahakama kwamba mshitakiwa ametoa maneno ya uchochezi. Pia alidai kuwa kesi zote zinazomkabili Lissu zimeletwa kuanzia mwaka 2016 na mpaka sasa hakuna hata moja iliyoisha ambapo zote zimetokana na mshitakiwa kupaza sauti. “Kutokana na kesi hizi upande wa serikali ndio unataka kumdhuru Lissu kwa kuwa anapopaza sauti, ndipo anakamatwa na suala la chuki kidini, Lissu ni Mkatoliki kama walivyo viongozi wengine wa serikali,” alidai Karume. Naye Wakili Peter Kibatala alidai upande wa mashitaka umeleta maombi hayo bila kuwa na hati ya kiapo na kwamba suala la ulinzi ni jukumu la serikali kumlinda mbunge ili asidhurike. Kibatala alidai upande wa mashitaka ulitakiwa kusema walimkamata Lissu Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere akielekea Kigali Rwanda kwenye mikutano wa mawakili. “Tunaomba apewe dhamana yenye masharti nafuu ili aweze kuyatimiza kwani hata alipokamatwa alikuwa ni mtu ambaye usalama wake haukuwa na mashaka,” alidai. Kutokana na hoja hizo, Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 27, mwaka huu kwa ajili ya kutoa uamuzi. Akisoma mashitaka hayo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi alidai mshitakiwa alitenda kosa hilo Julai 17, mwaka huu, maeneo ya Mtaa wa Ufipa Kinondoni, Dar es Salaam kwa kutoa maneno yenye chuki.

No comments