Kinyang'anyio cha uraisi bado cha endelea Kenya

Na Steven Charles kejo@kejonews.com.
Muungano wa upinzani nchini Kenya National Super Alliance (NASA) ulipomtangaza mgombea wake wa urais, na mgombea mwenza katika mkutano ukumbi wa Bomas Nairobi mwezi Aprili, kinyang'anyiro cha kipekee kilianza kujisuka. Kwa kumtangaza aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga kuwa mgombea mwenza na makamu wa rais wa zamani Kalonzo Musyoka kuwa mgombea mwenza wake, upinzani ulikuwa umehakikisha uchaguzi wa Agosti mwaka huu utakuwa kama marudio ya uchaguzi wa mwaka 2013. Bw Odinga, akitumia muungano wa Coalition for Reform and Democracy (Cord), wakiwa na Kalonzo, walishindana uchaguzini dhidi ya muungano wa Jubilee wake Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto. Wagombea wengine ni Cyrus Jirongo wa United Democratic Party (UDP), Ekuru Aukot wa Thirdway Alliance, Abduba Dida wa Alliance for Real Change (ARC), na wagombea huru Joseph Nyagah, Michael Wainaina na Japheth Kavinga. Wanachojiuliza watu ni iwapo kunafaa kutarajiwa matokeo tofauti na ya Machi mwaka 2013, Bw Kenyatta alipopata asilimia 50.7 ya kura, naye Bw Odinga akapata 43.31. Wanaoamini kwamba hakuwezi kutarajiwa matokeo tofauti, walikuwa miongoni mwa waliopinga Bw Odinga kuteuliwa kuwa mgombea wa muungano wa upinzani. Walitaka kuwe na mgombea tofauti ambaye 'angesisimua' upya hamu ya wapiga kura wenye imani na upinzani. Msimamo sawa, japo bila shaka kwa sababu tofauti, ulionekana kuwepo miongoni mwa mrengo wa serikali. Aliyeongoza ni Bw Ruto ambaye baada ya kutangazwa kwa mgombea wa upinzani, alisema: "Eti ile wametuletea ni ile ile ya 2013. Sasa, hii jameni ni utapeli wa aina gani. Sisi tulikuwa tunangojea walitwambia wako na maajabu, wako na miujiza. Tulikuwa tunafikiria wameenda kutoa mgombea nje ya nchi, kumbe ni wale wale tuliwashinda 2013. "Kama hawa, kwa sababu Raila ni yule yule, Kalonzo ni yule yule, Musalia (Mudavadi) ni yule yule .Hawa watu si tunawanyorosha asubuhi na mapema, hata kama ingewezekana tungewaambia sasa IEBC wasongeze uchaguzi ikuwe karibu," alisema akiwa mjini Thika. "Ni nini iliwazuia wangesema marudiano ya 2013 ni 2017, kivumbi tuliwaonyesha siku ile tutawaonyesha kivumbi pamoja na moshi." Walio na msimamo sawa, wanaamini safari itakuwa rahisi kwa Bw Kenyatta na wenzake kwani ukijumlisha kura alizopata Bw Odinga na zile alizopata Bw Mudavadi, ambayo sasa yumo kwenye muungano wa upinzani, hazitoshi kuwawezesha kuishinda serikali ya sasa. Bw Kenyatta alipata kura 6,173,433 naye Bw Odinga akapata 5,340,546 mwaka 2013. Bw Mudavadi alijizolea kura 483,981. Ukazijumlisha, Bw Kenyatta akiwa na 50.7, asilimia ya Bw Odinga na Bw Mudavadi kwa pamoja itakuwa ni 47.24. Lakini hali kwamba upinzani uliungana, tofauti na ilivyotarajiwa kwamba umoja wao ungesambaratika, unazua uwezekano kwamba kwa pamoja huenda wakafanya vyema kuliko awali.
Post a Comment